Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imepongeza uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli wa kuhamia Dodoma na kuahidi kuidhinisha kiasi cha dola za kimarekani milioni 455 (zaidi ya Sh 1.5 trilioni) kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa Msalato jijini Dodoma, sambamba na ujenzi wa barabara za mzunguko Jijini humo.
Rais wa AfDB, Dkt. Akinwumi Adesina ameyasema hayo katika Ofisi za Makao Makuu ya Benki hiyo jijini Abijdan nchini Ivory Coast wakati wa Mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi.
Dkt. Adesina ameongeza kuwa benki hiyo itaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Rais Dkt John Pombe Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Amesema Benki hiyo imeshaidhinisha kiasi cha dola za marekani milioni 180 kwa ajili ya ujenzi wa barabara za mzunguko jijini Dodoma na kwamba kiasi kingine cha dola za marekani milioni 275 kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Msalato kinatarajiwa kuidhinishwa mapema Novemba 2019.
Dkt. Adesina ameleza kuwa AfDB ina imani na mageuzi ya kiuchumi yanayotekelezwa chini ya Uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ikiwa ni pamoja na utoaji wa huduma za kijamii kama elimu bila malipo, afya, maji safi pamoja na mapambano dhidi ya rushwa.
Kwa upande wake Prof. Kabudi ameishukuru Benki hiyo kwa ushirikiano inaoutoa kwa Tanzania hususani katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli ambayo kimsingi yalikuwa ni maono ya Baba wa Taifa, Hayati Julius Kambarage Nyerere kwa nia ya kuiwezesha Tanzania kujitegemea kiuchumi na hatimaye bara zima la Afrika.
Prof. Kabudi ameongeza kuwa AfDB iko tayari kufadhili ujenzi wa reli ya kisasa yaani Standard Gauge Railway ya kipande cha kutoka Isaka hadi Kigali nchini Rwanda na kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mara baada ya kukamilika mchakato wa utoaji wa fedha hizo ambapo mazungumzo ya awali kuhusu ufadhili huo yameanza.
Prof. Kabudi yuko Abijdan nchini Ivory Coast kushiriki mkutano wa siku mbili wa dharura wa Mawaziri wa fedha uliondaliwa na AfDB.