Benki ya Maendeleo Afrika (AFDB) imesema itaiwezesha Serikali ya Tanzania ili ianzishe benki za wajasiriamali ambazo zitajikita katika kutoa mikopo kwa wahitimu wa mafunzo ya ufundi stadi na vijana wanaojihusisha na shughuli za kilimo.

Rais wa benki hiyo, Dk Adesina Akinumwi amemueleza hayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan wakati wa mazungumzo kati yao kwa njia ya simu, Ijumaa wiki hii, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa lengo la uanzishwaji wa benki hizo ni kusaidia juhudi za kupunguza tatizo la ajira kwa vijana na kuwasaidia kukua kiuchumi.

“AFDB itatoa ufadhili kwa Tanzania ili iweze kuanzisha benki za wajasiriamali zitakazotoa mikopo kwa vijana wanaohitimu mafunzo ya ufundi stadi na wanaojihusisha na shughuli za kilimo. Mikopo hii itawezesha kupunguza tatizo la ajira kwa vijana na kuwaongezea kipato,” amesema Dk Akinumwi.

Katika hatua nyingine, Dkt. Akinumwi amemueleza Rais Samia kuwa Benki hiyo itatenga Dola za Marekani bilioni 5 kwa ajili ya kuwasaidia wanawake. Viongozi hao wamekubaliana kuwa Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano wa uwezeshaji wa wanawake kiuchumi.

AFDB imeahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo.

Rais Samia azindua mtambo wa kutibu mfumo wa moyo
Mtuhumiwa Mbabe: Akata pingu akipelekwa hospitali, awazidi nguvu askari sita