Afisa wa kukatisha tiketi mjini Landon amefariki dunia baada ya kutemewa mate na mwanaume mmoja anayedaiwa kuwa alikuwa na maambukizi ya virusi vyacorona.
Belly Mujinga, 47 alikuwa kwenye kituo hicho tarehe 22 mwezi Machi wakati alipokabiliwa na mshukiwa huyo.
Mumewe Lusamba Gode Katalay amesema mwanaume huyo alimuuliza mke wake alikuwa akifanya nini pale.
”Alimjibu alikuwa kazini pale na mtu huyo akasema ana virusi kisha akamtemea mate,” ameeleza Katalay.
Shirikisho la wafanyakazi wa usafirishaji (TSSA) limesema Bibi Mujinga alilazwa hospitali ya Barnet tarehe 2 mwezi Aprili na kuwekwa kwenye mashine ya msaada wa kupumua, lakini alifariki siku tatu baadae.
BBC wameeleza kuwa Mujinga alikuwa na matatizo ya kupumua, alikuwa akifanya kazi katika kituo cha Victoria jijini London mwezi Machi alipodhalilishwa, sambamba na mfanyakazi mwenzie wa kike.
Ndani ya siku kadhaa baada ya tukio hilo, wanawake wote waliugua ugonjwa wa Covid-19.
“Alikuwa mtu mzuri, mama mzuri, na mke mzuri. Alikuwa mtu anayejali na angemtunza kila mtu.” ameeleza mumewake. Watu kumi walihudhuria mazishi ya Bi Mujinga, pamoja na binti yake wa miaka 11.