Watumishi wawili wa halmashauri ya mji wa Makambako mkoani Njombe wamekutwa na makosa ya utoro kazini baada ya mashauri yao ya kinidhamu kutolewa uamuzi na baraza la madiwani na kupelekea mmoja kusimamishwa kazi huku mwingine akipewa onyo na kukatwa mshahara wake 15% kwa muda wa miaka mitatu.
Akitangaza maamuzi hayo Makamu mwenyekiti wa halmashauri ya Mji wa Makambako Salum Mlumbe amewataja watumishi hao kuwa ni Boniface Kyando ambaye ameonywa na kusalia kazini na ofisa muuguzi msaidizi wa zahanati ya kitisi Frank Thomas Selestin akifutwa kazi.
“Tumepitia na tumejiridhisha hatimaye tumetoa maamuzi,Boniface Kyando ni mtendaji wa mtaa wa Golgota kata ya Kitisi huyu anabaki kazini lakini atakatwa mshahara wake asilimia kumi na tano kwa muda wa miaka mitatu kwa kosa la utoro kazini”alisema Mlumbe
“Wa pili ni bwana Frenk Thomas Selestin ambaye ni afisa muuguzi msaidizi daraja la pili katika zahanati ya Kitisi,kosa lake ni utoro kazini tunamfukuza kazi kuanzia leo”
Aidha Makamu mwenyekiti amemtaka mkurugenzi wa halmashauri kukutana na watendaji wote ili kuwakumbusha majukumu yao ya kazi ili watekeleze kwa weledi na halmashauri iweze kufikia malengo waliyojiwekea ikiwemo Ukusanyaji wa mapato.
Akirejea maagizo ya maagizo ya mkuu wa wilaya,Makamu mwenyekiti wa halmashauri amekiri kuwa mapato ndiyo uhai wa halmashauri hivyo amesisitiza ushirikiano baina ya mkurugenzi na madiwani katika kufikia malengo yaliyokusudiwa.