Kuna ule usemi kwamba Mvumilivu hula mbivu na pia mchumia juani hulia kivulini lakini bado wahenga wakaongeza mchuma janga hula na wa kwao. Semi hizi zote zina maana kila moja kwa namna yake ingawa inapotokea mtu akavumilia sana hasa kwa maisha ya sasa wengi uvumilivu huwaishia na kuamua kuchuma majanga.
Vipo vitu ambavyo wasaikolojia wanaviorodhesha kama sababu za wanaadamu wengi kufikia maamuzi ya kujitoa uhai na vyote hivi ni katika hali ya kubanwa na mawazo ikijulikana kama Msongo. Je ni vitu gani vinavyoweza kukusababishia wewe upate fikra za kujitoa uhai?
Afisa wa polisi kutoka kijiji cha Koromotangi kaunti ya Kakamega nchini Kenya amejitoa uhai kutokana na msongo wa mawazo uliotokana na madai ya kucheleweshwa kwa mshahara.
Ripoti zinaonyesha kuwa afisa huyo aliyetambuliwa kwa jina Abel Kemboi alipatikana Jumatano, Januari 5, akiwa amefariki dunia baada ya kuwalalamikia wenzake kuhusiana kucheleweshwa kwa mshahara.
Afisa hiyo aidha alikuwa amesema atafuatilia swala la mshahara na wakuu wake katika kituo cha polisi cha Kakamega na hata akamuomba binamu yake Zacheaus Kalama kuongozana naye.
“Tulikuwa tumekubali kwenda kituoni kuuliza sababu ya kucheleweshwa kwa mishahara kutoka kwa wakubwa wake lakini ilishangaza kwamba alijitoa uhai hata kabla hatujatimiza dhamira yetu,” Kalama alisema.
Kalama alisema kwamba aliamka asubuhi iliyofuata na kuelekea nyumbani kwa Abel lakini akakuta mlango umefungwa kwa ndani. Juhudi za kumtaka afungue mlango ziliambulia patupu hivyo kuamua kuingia ndani ya nyumba hiyo na ndipo alipomkuta Abel akiwa amejitoa uhai.
“Alikuwa amejinyonga na sikuamini nilichokiona,” Kalama alisema huku akifichua kwamba binamu yake hata hivyo alionyesha dalili za kuzongwa na mawazo siku za hivi karibuni. Aidha bosi wake wa karibu OCPD wa Kakamega ya Kati David Kabena alidhibitisha kwamba ni kweli marehemu alikuwa akitatizwa kiakili mara kwa mara.
Alisema kuwa tayari wameanzisha uchunguzi kubaini chanzo hasa cha kifo chake huku akiwataka maafisa wenye matatizo yoyote ya kiakili kutafuta usaidizi wa kitaalamu. “Ni muhimu kwa wale wanaotambua kwamba wana msongo wa mawazo kujieleza na kutafuta kusaidiwa,” Kabena alisema.
Mwili wa Abel ulipelekwa katika chumba cha maiti cha hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Kakamega ukisubiri kufanyiwa upasuaji na kugundua zaidi juu ya chanzo.