Kocha wa zamani wa Simba SC, Patrick Aussems amefichua kuwa kama kweli Simba SC wanataka kufuzu hatua ya Nusu Fainali katika michuano ya Africa Football League ‘AFL’ basi wachezaji wake wakiwemo Mzambia, Clatous Chama na Mrundi, Saido Ntibanzokiza wanapaswa kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu dhidi ya Al Ahly kutoka Misri.
Aussems raia wa Ubelgiji, ametoa kauli hiyo kuelekea katika mchezo huo wa uzinduzi wa michuano hiyo inayozinduliwa leo jijini Dar kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.
Simba SC itacheza mchezo huo ikiwa imeingia kwenye rekodi ya klabu ya kwanza Tanzania na Afrika Mashariki na Kati kuwepo katika michuano hiyo huku ikipewa nafasi kubwa ya kushinda mchezo wa ufunguzi unaotarajia kupigwa leo Ijumaa (Oktoba 20).
Aussems amesema kuwa hawezi kumpangia kocha wa timu hiyo Robertonho Oliviera cha kufanya kwa kuwa na mikakati yake kwenye michuano hiyo lakini anaweza kuwaambia wachezaji wa timu hiyo kuhakikisha wanacheza kwa nidhamu kubwa ya kuweza kuwapa matokeo katika mchezo huo.
“Naona Simba SC wana nafasi kubwa ya kushinda mchezo wa kwanza na kuandika rekodi mpya kwa sababu hawana ugeni wa kucheza na Al Ahly kwa sababu wameshacheza mara kadhaa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na Simba SC ikapata matokeo nyumbani, na siwezi kusema kiufundi mchezo utakuwaje kwa kuwa mwalimu ndiyo anatambua mipango yake.
“Lakini ninachoweza kusema ni juu ya wachezaji kutambua umuhimu wa mchezo wenyewe kwa timu pamoja na nchi na kwa nini wanatakiwa kupata matokeo ya ushindi, wanatakiwa wacheze kwa nidhamu kubwa sana na kutumia vizuri uwanja wa nyumbani, naelewa timu inavyokuwa ikiwa na mchezo wa aina hii lakini umakini pekee ndiyo unaweza kuwavusha,” amesema Aussems.