Bara la Afrika limeendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa chakula, viwango vikubwa vya ukosefu wa ajira, umaskini uliokithiri na ukosefu wa usawa kwenye jamii, licha ya harakati mbalimbali za ukuzaji wake wa Uchumi.
Hayo yamebainishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan hii leo Julai 26, 2023 wakati akizungumza kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Rasilimali Watu Jijini Dar es salaam na kusema ni wazi kuwa bado mageuzi makubwa yanahitajika katika nyanja zote muhimu za uzalishaji na maendeleo.
Amesema, “na hayo ndio malengo na madhumuni ya agenda ya Maendeleo ya Afrika tunayoitaka ya mwaka 2063, ambayo imeweka malengo saba na hapa najielekeza kuzungumzia malengo manne ambayo ni Africa ambayo mafanikio yake yanajikita kwenye ukuaji Jumuishi wa uchumi na maendeleo endelevu.”
Rais Samia amesema inahitajika Africa yenye utengamano kisiasa kwa kuzingatia fikra za kimajumui na mwelekezo wa kimapinduzi, misingi ya utawala bora wa demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria na ambayo maendeleo yake yanatokana na watu.