Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis amewasili nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo – DRC, kuanza ziara itakayoangazia athari za mzozo wa muda mrefu, kwenye taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa madini.
Papa Francis anakuwa ni kiongozi wa kwanza wa kanisa hilo kutembelea DRC, tangu Papa John Paul II alipozuru nchi hiyo mwaka 1985, wakati huo ikiitwa Zaire ikiwa na karibu nusu ya idadi ya watu karibu milioni 90 ambao ni Wakatoliki.
Ujumbe wa Papa Francis, umewasili jijini Kinshasa kwenye ziara hiyo inayoelezewa kuwa ni ya amani na ikilenga kukabiliana na dhana ya kikoloni kwamba bara la Afrika liko tayari kunyonywa kama ambavyo inasemekana.
Mara baada ya kumaliza ziara katika jiji la Kinshasa siku ya Ijumaa (Februari 3, 2023), Papa Francis ataelekea mjini Juba nchini Sudan ya Kusini kabla ya kurejea Vatican siku ya Jumapili Februari 5, 2023.