Afrika Kusini imerejesha hatua kali za kuzuia maambukizi ya virusi vya corona kwa kupiga marufuku mikusanyiko, kutotoka nje usiku na uuzaji wa pombe kutokana na ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona kufikia Milioni moja
Wizara ya Afya nchini humo imetangaza iko katikati ya wimbi la pili la maambukizi, huku zaidi ya visa milioni moja vya covid-19 vimesajiliwa tangu mwezi Machi.
Katika hotuba yake kwa taifa aliyoitoa kwa njia ya televisheni, Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, ametangaza kurejeshwa kwa hatua za kukabiliana na maambukizi zilizoanza mara moja.
Kama ilivyo kwa Uingereza, Afrika Kusini inapambana na aina mpya ya kirusi cha Corona, ambacho wataalamu wanadai kwamba kinasambaa zaidi kuliko cha hivi sasa.
Chama cha wafanyakazi wa afya cha Afrika Kusini kinachowakilisha wauguzi na madaktari, kimeonya kwamba mfumo wa afya wa taifa hilo uko karibu kuzidiwa na mchanganyiko wa idadi kubwa ya wagonjwa wa Covid-19 na wagonjwa wengine wanaohitaji huduma ya dharura.