Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Afrika na Mawaziri wa nchi za Nordic wamekubaliana kuimarisha biashara na uwekezaji, kubadilishana ujuzi, teknolojia pamoja na kukuza uwekezaji baina ya nchi hizo wakati wa Mkutano wao 20 unaoendelea Jijini Algiers, Algeria ulioanza Oktoba 16, 2023.
Akizungumza baada ya makubaliano hayo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba amesema kuwa mkutano huo umekuwa na mazungumzo ya tija kuhusu ushirikiano wa kuimarisha biashara na uwekezaji kati ya Afrika na nchi za Nordic, kubadilishana ujuzi, teknolojia pamoja na kukuza uwekezaji.
Amesema, “tumekuwa na mazungumzo yenye tija yanayolenga kuimarisha biashara na uwekezaji kati ya nchi Afrika na nchi za Nordic, kubadilishana ujuzi, na teknolojia pamoja na kukuza uwekezaji baina ya nchi zetu, katika mkutano huo, Mawaziri wa nchi za Afrika na Nordic tumekubaliana kufanya kazi kwa bidii, ili kuchochea ongezeko la uwekezaji.”
Awali akifungua Mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria, Ahmed Attaf alisema kuwa Afrika inaendelea kujizatiti kuimarisha zaidi ushirikiano wake na nchi za Nordic kwa maslahi mapana ya pande zote hususan katika vipaumbele kwenye masuala ya amani na usalama, biashara na uwekezaji na elimu ya ufundi, ili kuwawezesha vijana kupata ujuzi na maarifa.
Akiongea kwa niaba ya Nchi za Nordic, Waziri wa Mambo ya Nje wa Denmark, Lars Løkke Rasmussen alisema kuwa Nordic itaendelea kushirikiana na Umoja wa Afrika (AU) na Afrika kwa ujumla katika kuhakikisha kuwa amani na usalama vinaendelea kudumishwa.
Aidha, mkutano huo pia umejadilia masuala ya ulinzi na usalama hususan kwenye mapambano dhidi ya ugaidi na mageuzi katika Umoja wa Mataifa; kuweka mikakati ya kuboresha elimu Barani Afrika; kukuza biashara na uwekezaji baina ya pande mbili na umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kimataifa ili kukabiliana na changamoto zinazoikabili dunia kwa sasa ambazo zinahitaji ushirikiano ili kuzitatua.