BARA la Afrika limeunga mkono pendekezo la fainali za Kombe la Dunia kuandaliwa kila baada ya miaka miwili licha ya kwanza tayari Shirikgisho la Soka la Afrika (CAF) huandaa kampeni za Kombe la Afrika (AFCON) kila baada ya miaka miwili.
Patrice Motsepe ambaye ni rais wa CAF, ameunga mkono mpango wa kubadilishwa kwa ratiba ya sasa ya Kombe la Dunia kam ilivyopendekezwa na Saudi Arabia kwenye kikao kikuu cha Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) mnamo Juni 2021.
“Kamati Kuu Tendaji ya CAF imeridhishwa na pendekezo hilo na inaunga mkono mpango huo kikamilifu,” amesema Motsepe Julai 17 kwenye mkutano mkuu wa Kamati Kuu ya CAF nchini Morocco.
Kwa mujibu wa CAF, hatua ya kuandaliwa kwa fainali za Kombe la Dunia kila baada ya miaka miwili, itashuhudia FIFA ikipata mapato zaidi kutokana na mashindano hayo ambayo kwa sasa hufanyika kila baada ya miaka minne.
Hata hivyo, Motsepe alishindwa kufafanua jinsi Afrika itakavyomudu kushiriki Kombe la Dunia na AFCON pamoja na kushiriki mechi za kufuzu kwa vipute hivyo kila baada ya mwaka mmoja.