Viongozi wa Mataifa mbalimbali barani Afrika wameendelea kutuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli aliyefariki dunia jana Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam alikokuwa anapatiwa matibabu.
Miongoni mwao ni pamoja na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, Rais wa Uganda Yoweri Museveni na Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa.
Raisi wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, ameeleza masikitiko yake kufuatia kifo cha Rais wa Tanzania, John Magufuli.
Katika taarifa yake, Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa ameeleza kusikitishwa na taarifa za kifo cha Rais Magufuli akisema amezungumza na Makamu wa Raisi, Samia Suluhu Hassan akimweleza huzuni yake na kwa niaba ya raia wa Afrika Kusini.
‘’Afrika Kusini inaungana na Serikali na watu wa Tanzania katika kipindi hiki kigumu,’’ amesema Ramaphosa.
Naye Rais wa Uganda, Yoweri Mseveni katika salamu za rambirambi alizotuma kupitia ukurasa wake wa Twitter, amesema amesikitishwa sana na kifo cha Rais Magufuli.
Museveni amemuelezea Magufuli kuwa kiongozi aliyeongoza kwa uhalisia na aliyeamini katika kukuza uchumi wa Afrika Mashariki.
“Tunajumuika na Watanzania kuomboleza kifo cha mtoto wa Afrika.
Roho yake ipumzike kwa amani,” ameandika Museveni.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari akituma salamu zake za rambirambi, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya na Kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, amemtaja Magufuli kama kiongozi aliyejaribu kuimarisha hali ya raia wa Tanzania.
Odinga amesema kuwa Rais Magufuli amekuwa rafiki yake wa muda mrefu na kwamba amekuwa kando yake wakati mgumu alipomuhitaji na kwamba tangazo la kifo chake amelipokea kwa a huzumi kubwa akiongeza kwamba anasimama na familia ya marehemu wakati huu wa maombolezo.
Kiongozi huyo amesema kwamba kwa miaka kadhaa iliyopita ameshirikiana na rais Magufuli haswa katika kuiunganisha Afrika mashariki kupitia miundombinu.
Odinga amewataka Watanzania wote kuwa watulivu na kufuata utamaduni ulioachwa na Rais wa Kwanza na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyererena wa viongozi waliofuata katika kukabidhiana mamlaka kulingana na Katiba ya Tanzania.