Jumla ya chupa 100 za damu zimekusanywa katika Warsha ya ‘’Afya Day’’ iliyoratibiwa na Wizara ya Afya, Idara ya Kinga, Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma na kufanyika katika chuo Kikuu cha Mtakatifu Yohane (St. John University), jijini Dodoma.

Akizungumza katika ufungaji wa hafla hiyo ya “Afya Day”, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma, Dkt. Tumaini Haonga amesema jumla ya wananchi 138 walijitokeza kuchangia damu wakati wa tukio hili ambapo matarajio yalikuwa ni kukusanya chupa hizo 100.

Amesema, “Tunaweza kuhudumia wagonjwa 130 kwa kuwapa damu kwa awali ,kwa niaba ya Wizara ya Afya nawashukuru sana kwa kuwa na utashi huu kwa sababu kupitia matukio haya tunaonesha kwa vitendo kwa wanafunzi wanaosomea sekta ya Afya.”

Kuhusu mwelekeo wa Wizara, Dkt.Haonga amehimiza umuhimu wa Bima ya afya kwa wote katika kuleta unafuu wa matibabu na kurahisisha ubora wa huduma kwa kila mwananchi huku Afisa Mpango wa Taifa, Huduma za Afya ngazi ya Jamii, Wizara ya Afya, Mwailafu Bahati akisema katika tukio hilo, watu 277 wamepatiwa elimu ya Afya pamoja na ushauri nasaha.

Amesema, “Katika tukio hili watu 277 wamepata elimu ya afya,waliopata huduma ni 241,waliopima msukumo wa damu ni 110,shinikizo kubwa la damu 11 huku mmoja akigundulika na shinikizo dogo la damu,waliopima uzito ni 157 na 34 wakigundulika kuwa na uzito mkubwa.”

Kwa upande wake Mratibu wa mpango wa taifa wa Afya Shuleni, Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma, Idara ya Kinga, Wizara ya Afya, Beuaty Mwambebule amewahimiza vijana kujihusisha masuala ya Elimu ya Afya huku Rais wa serikali ya Wanafunzi Chuo Kikuu cha St. John, Alicia Mwami akizungumzia manufaa ya Afya Day kuwa ni pamoja na kupima na kupata elimu ya Afya.

Fiston Mayele awaita Wananchi kwa Mkapa
Doumbia achimba mkwara Young Africans