Waziri Mkuu, Kassim Mjaliwa ameiagiza Wizara ya Nishati kuhakikisha inaratibu utekelezaji wa agizo lililotolea na Rais wa awamu ya tano Hayati John Magufuli, la mikoa ya kanda ya kaskazini kuagiza mafuta kutoka ghala la kampuni ya GBP lililopo Jijini Tanga.
Majaliwa ametoa agizo hilo akiwa katika ziara ya siku moja jijini humo ambapo pia alitembelea ghala la kuhifadhi mafuta ya Petroli, Dizel na ya Taa.
Amesema, “haiwezekani Mtanzania afanye uwekezaji mkubwa kama huu halafu tumkatishe tamaa kwa kushindwa kusimamia wanunuzi kuja Tanga kununua mafuta, Wizara ya Nishati na Taasisi zake zinazosimamia nishati naagiza kwa mara nyingine malalamiko haya iwe ni mwisho.”
Aidha, Majaliwa amesema Serikali itaendelea kutoa fedha kwaajili ya uwekezaji mkubwa wa upanuzi wa bandari iweze kumudu shehena kubwa kwa haraka, ambapo alitembelea bandari hiyo na kushuhudia maendeleo ya mradi wa uchimbaji wa kina na uapnuzi wa gati ambao utagharimu bilioni 429. 2 hadi kukamilika.
Naye, Naibu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania – TPA, Juma Kajavala alisema awamu ya kwanza ilikuwa ya uchimbaji wa kina kutoka mita 3 hadi kufikia mita 13 na awamu nyingine ilikuwa ya upanuzi wa gati hadi kufikia 450 ndani ya maji hivyo kuiwezesha bandari kupokea na kuhifadhi shehena nyingi kwa wakati mmoja.
Awali akimkaribisha Waziri Mkuu, Mbunge wa Tanga, Ummy Mwalimu alisema licha ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na GBP wa kujenga ghala la kupokea, kuhifadhi na kusambaza mafuta nchini na nchi za ukanda wa maziwa makuu wanunuzi wa mikoa ya kanda ya kaskazini bado wananunua mafuta yanayoagizwa kupitia bandari ya Dar es Salaam.
” Hii inatuumiza sana sisi watu wa Tanga licha ya Rais John Magufuli kutembelea ghala hili na kuagiza wanunuzi wa mikoa ya kanda ya kaskazini kununua mafuta kutoka Tanga kwasababu ni karibu utekelezaji wake unasuasua serikali inatakiwa kuingia kati” Alisema Ummy.