Mwanaharakati wa nchini Uganda, Stella Nyanzi ambaye pia ni mwanazuoni, mwishoni mwa wiki hii aligoma kutoka mahabusu kwa dhamana akitaka abaki ndani hadi kesi yake itakaposikilizwa.
Nyanzi ambaye anashtakiwa kwa kosa la kumdhihaki na kumtusi marehemu mama yake Rais Yoweri Museveni kupitia Facebook, amedai kuwa anataka kubaki ndani ya magereza ili awafundishe wafungwa namna ya kutumia mtandao huo wa kijamii.
“Ni nini ambacho wanaendelea kuchunguza hadi sasa-bado wanataka kujua kama Yoweri Museveni alidhihakiwa? Nitaendelea kuwa na wale wanawake huko Luzira (gerezani) niwafundishe jinsi ya kutumia na kuandika kwenye Facebook,” Nyanzi anakaririwa na vyombo vya habari nchini humo akiwa eneo la Mahakama baada ya kuambiwa dhamana yake iko wazi.
“Nataka wale wanawake wa gerezani nao wakiachiwa waweze kujua namna ya kuandika kwenye Facebook kadiri wawezavyo. Kama mwandishi, mshairi… ninapoandika kwa ajili ya watu wengi, ninaandika kukosoa utawala,” aliongeza.
-
Picha: Polisi waonesha nyumba aliyofichwa Mo Dewji alipotekwa
-
Bobi Wine afanya tamasha la kwanza tangu ashtakiwe
Nyanzi sio mgeni kwenye harakati zinazomtia matatani nchini humo, alikamatwa mwaka jana na kufunguliwa mashtaka kwa makosa ya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii. Alidaiwa kutumia mtandao huo kumtukana Rais. Mashtaka hayo dhidi yake yalifutwa na akaachiwa huru.
Mwanaharakati huyo amerudishwa rumande hadi Novemba 22, kesi yake itakapoanza kusikilizwa.