Beki na Nahodha wa Azam FC Agrey Morris amesema alitimiza jukumu lake kwa kumkaba Mshambuliaji hatari wa Young Africans Fiston Kalala Mayele kwenye mchezo uliozikutanisha timu zao jana Jumatano (April 06), Uwanja wa Azam Complex, Chamazi-Dar es salaam.
Azam FC ilipoteza mchezo huo kwa kufungwa mabao 2-1, huku ikitangulia kupata bao kupitia kwa Mshambuliaji wake Rodgers Kola, kabla ya Beki wa pembeni wa Young Africans Djuma Shaban hajawasazisha kwa mkwaju wa Penati na Mshambuliaji Fiston Mayele kufunga bao la pili na la ushindi.
Agrey amesema anaamini alifanya kazi yake ipasavyo licha ya Mshambuliaji huyo kuifungia Young Africans bao la ushindi kwa kupiga mpira kiufundi uliojaa langoni mwa Azam FC bila ajizi.
“Kwangu nimetimiza wajibu wangu kama Beki, nilifanya nilivyoagizwa na kilichotokea ni sehemu ya majukumu yake kama Mshambuliaji, hivyo kufunga kwake kusichukuliwe kama sehemu ya mimi kushindwa kumkaba.”
“Hatukua na ugomvi wowote japokuwa Mwamuzi wakati fulani alikua akitusisitiza kucheza kwa umakini na kiungwana zaidi, wakati mwingine mimi na yeye tulikua tukicheka, ila sikuzungumza naye lolote kwa sababu nilikua kazini.” amesema Agrey.
Katika hatua nyingine Agrey Morris amekipongeza kikosi cha Young Africans kwa kupata matokeo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi-Dar es salaam na kuwatakia kheri kwenye mbio za kusaka ubingwa msimu huu.
“Nipende kuwapongeza kwa kushinda hapa Azam Complex, pia ninawatakia kheri kwenye harakati zao za kuwania ubingwa msimu huu.” amesema beki huyo.
Ushindi dhidi ya Azam FC unaiwezesha Young Africans kufikisha alama 51 baada ya kucheza michezo 19, na kuwaacha Mabingwa Watetezi Simba SC iliyocheza michezo 17 kwa alama 11, huku Azam FC wakisalia na alama 28.