Katibu Mkuu wa wizara ya maji, Prof.Kitila Mkumbo amezindua ujenzi wa mradi mkubwa wa maji wa zaidi ya nshilingi bilioni 15.1 utakao sambaza maji kwenye miji ya Kyaka Na Bunazi kwa kuwahudumia wananchi zaidi ya elfu 50 ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa Rais John Magufuli wakati wa ziara yake mwezi julai 2019, wilayani missenyi Mkoani Kagera.
Katibu mkuu amesema kuwa wizara ya maji imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maji hapa nchini ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama cha mapinduzi.
Kitila amesema Rais Magufuli alipofika Kyaka akitokea Karagwe alipokea kilio cha wananchi wa wilaya hiyo ambnao walimuomba kuwatatulia kero ya maji ambayo imekuwa ni kero ya kudumu tangu inchi inapata uhuru na ndipo aliahidi kuwajengea mradi mkubwa wa maji na sasa utekelezaji wake utaanza mara moja.
Ameongeza kuwa wizara kupitia Mamlaka ya maji na usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) imengia mkataba na mkandarasi kampuni ya China Civil Engineering contractions corporation ambapo amesema kuwa mradi wa maji Kyaka-Bunazi utagarimu shilingi Bilioni 9.4.
“Fedha kwaajili ya utekelezaji wa mradi huu zinatolewa na Serikali ya Tanzania kupitia mfuko wa maji, hivyo kwadhati kabisa ninachukua fursa hii kwaniaba ya wizara ya maji pamoja na wakazi wote wa Kyaka-Bunazi kumshukuru Rais Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya kuhakikisha anamtua mama ndoo kichwani.” Amesema Prof.Kitila.
Aidha amezitaka mamlaka za wilaya ya Missenyi chini ya mkuu wa wilaya na kamati ya ulizi na usalama kuhakikisha wanafatilia mradi huo kwa ukaribu na kwa kila hatua ili agizo Rais kutekelezwa kwa wakati na ukamilifu.
Akiongea kwa niaba ya wananchi wa wilaya missenyi, mwenyekiti wa halmashauri hiyo Projestus Tegaamaisho amesema kuwa wananchi wa wilaya hiyo wanachangamoto kubwa ya maji hali inayowapelekea wanaume kuamka asubuhi sana kwenda kuchota maji kwenye mito ambayo pia sio salama ili kuwasaidia wake zao na wengine kulazimika kununua maji kwa gharama kubwa.
Ameongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo utawasaidia sana wananchi kuachana na kero ya maji hasa wa miji ya Kyaka na Bunazi ambao maisha yao yote hutegemea maji ya chumvi na wengine maji ya mto Kagera ambayo sio salama kwa afya zao.
Katika hatua nyingine katibu mkuu amemwagiza mkandarasi kuhakikisha anatoa ajira kwa vijana wa wilaya ya missenyi wakati wote wa utekelezaji wa mradi huu kwa shughuli zote ambazo sio za kitaalamu zaidi ili iwe fursa kwa wakazi wa missenyi, na kutoa wito kwa wananchi ambao mradi huu utakuwa unapita kwao wapishe mradi na wasiwe chanzo cha kukwamisha mradi.