Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema anayeungwa mkono na Ukawa, Edward Lowassa amesema endapo atachaguliwa kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, vivuko vyote vilivyoko nchini vitatoa huduma bure.

Lowassa aliitoa ahadi hiyo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akifanya mkutano wa kampeni katika eneo la Kigamboni baada ya kupokea maelezo ya kuwepo changamoto ya usafiri huo.

Mgombea huyo alisisitiza kuwa serikali ya Chadema itaanza kutekeleza ahadi hiyo wiki moja baada ya kuingia madarakani.

“Nimemsikia Mbowe akieleza habari ya Ferry…nawaambia hivi, tarehe 25 Oktoba, mkishanichagua, Jumatatu inayofuata ni suala la ferry. Ferry ni lazima iwe bure,” alisema Lowassa na kushangiliwa na wananchi waliohudhuria katika mkutano huo.

Lowassa na timu ya Ukawa walisisitiza kuwa vivuko vyote nchi nzima vitakuwa vikitoa huduma bure.

Aidha, Lowassa aliwaahidi wakazi wa Kigamboni kuwa serikali yake itakuwa rafiki kwa wafanyabiashara wadogo wakiwemo mama ntilie na bodaboda ikiwa ni pamoja na kuanzisha benki maalum kwa ajili ya wafanyabiashara hao.

Mgombea huyo, alifanya ziara yake jijini Dar es Salaam ambapo alifanikiwa kufanya mikutano mitatu katika eneo la Ukonga, Mbagala na Kigamboni.

Magufuli: Shukurani Ya Punda Ni Mateke
Serikali Ya Magufuli Kushusha Meli Tano Bahari ya Hindi