Meneja wa Habari na Mawasilino Simba SC Ahmed Ally amehimiza Umoja na Mshikamano kwa Wanachama na Mashabiki wa Klabu hiyo kuelekea mchezo wa Mzunguuko watano wa Kundi C, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Horoya AC.
Simba SC itawakaribisha Mabingwa hao wa Guinea Jumamosi (Machi 18), katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku mnyama akihitaji ushindi ili kujihakikishia kutinga Robo Fainali, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Ahmed Ally amesema Simba SC inahitaji ushindi kwa hali na mali kwenye mchezo huo, hivyo kila Shabiki na Mwanachama anapaswa kuitanguliza kwanza klabu hiyo, na kuachana na mambo mengine ambayo huenda yakawavurugia mambo.
Ahmed amesema amaamini Simba SC ipo shwari, lakini umakini wa kila mmoja katika kipindi hiki utaendelea kuongeza chachu ya kupata ushindi kwenye mchezo huo, ambao umepangwa kuchezwa kuanzia saa moja usiku.
Amesema kuwa wanakumbuka walipoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Horoya AC wakiwa ugenini, kisha wakapoteza nyumbani dhidi ya Raja Casablanca ya Morocco, hali ambayo iliwafanya baadhi ya Mashabiki na Wanachama kujitenga na kuanza kusema wana kikosi dhaifu, lakini ushindi dhidi ya Vipers SC umerudisha Umoja na Mshikamano ambao anaamini kama utadumishwa, basi Horoya AC anakufa kwa kupigwa kitu kizito.
“Kila mchezaji alikuwa anahitaji ushindi kwenye mchezo wa kwanza na hata benchi la ufundi pamoja na mashabiki lakini mpira ulitukatili na tukapoteza sasa wanakuja Dar hakika watakutana na kitu kizito ambacho ni kuacha alama tatu.”
“Sisi hatuna matatizo hasa baada ya kupoteza dhidi ya Raja Casablanca tukakubaliana kushinda michezo yetu miwili na kukusanya alama sita hizi ni muhimu na tumeanza na Vipers kisha wao wanafuata, ambao ni Horoya AC.”
“Mashabiki tunawaomba mzidi kuwa pamoja nasi kwa kuwa wamekuwa pamoja nasi katika kazi hizi ambazo tunafanya, tunatambua wachezaji wapo tayari hivyo wazidi kuwa pamoja nasi bega kwa bega.”
Katika msimamo wa Kundi C la Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, Simba SC inakamatia nafasi ya pili ikiwa na alama sita, katika michezo minne waliyocheza wakishinda michezo miwili na kupoteza michezo miwili.” amesema Ahmed Ally
Raja Casablanca wanaongoza msimamo wa Kundi hiyo kwa kufikisha alama 12, ambazo zinawawezesha kufuzu moja kwa moja hatua ya Robo Fainali, huku Horoya AC ikiwa nafasi ya tatu kwa kuwa na alama 04 na Vipers SC inaburuza mkia kwa kuwa na alama 01.