Uongozi wa Simba SC umesikia vilio vya baadhi ya Mashabiki wa Young Africans vilivyosikika baada ya kikosi chao kushindwa kufurukuta mbele ya Al Hilal ya Sudan katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika mwishoni mwa juma lililopita (Oktoba 08).

Young Africans ililazimishwa sare ya 1-1 Uwanja wa Benjamin Mkapa, hali ambayo ilipelekea Mashabiki wa Klabu hiyo ya Jangwani kusisitiza Uongozi wao umeshindwa kutimiza wajibu wa kupambana katika Uwanja wa nyumbani, tofauti na wanavvyofanya wenzao wa Simba SC.

Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema wamesikia vilio vya Mashabiki wa Young Africans, lakini amewarekebisha kwa kusema wao hawatumii njia za mkato kushinda nyumbani kwenye Michuano ya Kimataifa, zaidi ya kujiandaa na kupambana kwa malengo.

“Tumewasikia wakisema sisi huwa tuna mipango ya kabla ya mchezo wetu wowote wa Kimataifa, lakini ukweli ni kwamba sisi tunajiandaa kwa malengo, na tukipambana tunapambana kwa malengo tuliojiwekea, hatutumii njia za mkato kama wanavyofikiria.”

“Nikupe mfano, Simba SC ndio timu pekee Tanzania iliyojiandaa na michuano ya Kimataifa wakati wa Pre Season, tulikwenda Misri kujiandaa na Michuano hii, hatukwenda Misri kwa ajili ya kumfunga Mtibwa, Ihefu ama yoyote yule, tulikwenda kujiandaa kwa ajili ya Michuano ya Kimataifa.”

“Wenzetu wamekua na kasumba ya kijiandaa kuifunga Simba SC kwa sababu wanaamini hilo ndio lengo lao kubwa kwa kila msimu, sasa ukitazama hapo kuna tofauti kubwa sana kati yetu na wao, niwasisitize kuwa Simba SC tunajiandaa hatupiti njia za mkato jamani.” amesema Ahmed Ally

Simba SC imepiga hatua moja kuelekea hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu 2022/23, kufuatia ushindi wa 3-1 dhidi ya Primeiro De Agosto ya Angola, huku ikitarajia kucheza mchezo wa Mkondo wa Pili Jumapili (Oktoba 16), Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Kocha Nabi abadilisha DOZI Young Africans
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Octoba 12, 2022