Licha ya kupigwa vita na upande wa Young Africans kuhusu mpango wa kuwahamasisha Mashabiki wa Simba SC wakati wa maandalizi ya Mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Orlando Pirates, Meneja wa Habari na Mawasilino wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Ahmed Ally ameibuka na kusisitiza alikua sahihi kutumia njia ya kuwafikia Mashabiki mitaani na kwenye Matawi yao.
Ahmed Ally pamoja na baadhi ya Viongozi wa Simba SC walifanya hivyo kwa siku kadhaa za juma, ili kufanikisha lengo la kila shabiki wa klabu hiyo kufika Uwanja wa Benjamin Mkapa, kuipa nguvu timu yake iliyohitaji kuhamasishwa ndani ya dakika 90, ili itimize mpango wa kuibuka na ushindi.
Ahmed ametumia ukurasa wake wa Instagram kufanya msisitizo wa mpango alioutumia, kwa kulinganisha na walivyofanya baadhi ya viongozi wa klabu ya Mamelod Sondown ya Afrika Kusini walipokua kwenye maandalizi ya kuelekea Mchezo wa Mkondo wa Pili wa Robo Fainali Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Petro Atletico ya Angola.
Ahmed anaamini Simba SC ilitumia njia sahihi ambayo pia ilitumiwa na Uongozi wa Mamelod Sundown inayosifika kuwa na uwekezaji wa kutoka miongoni mwa klabu za BArani Afrika.
Ahmed ameandika: Kuelekea mchezo wao wa Robo Fainali dhidi ya Petro Atletico klabu ya Mamelod Sundown walifanya Road Shows
Walienda kwenye maduka makubwa (Tembisa Mall na Maponya Mall) wakiwa wameambatana na wachezaji na viongozi wajuu wa klabu
Mashabiki walipata fursa ya kupiga picha na wachezaji wao na viongozi walitumia fursa hiyo kuuza Tiketi na kuutangaza mchezo wao
Hapa wamefanya vitu viwili kwanza Match Promotions na pili ni Fans Engagement
Hivi ni vitu muhimu sana kwa Biashara ya mpira hasa Africa ambako bado kuna tatizo la watu kuhudhuria viwanjani
Kwa kiasi kikubwa Simba tumepiga hatua kwenye Promotions na Fans Engagement lakini tunaendelea kujifunza kutoka kwa wengine na tunaendelea kubuni njia mbalimbali za Promo na Engagement
Lengo letu ni kutengeneza kizazi chenye kupenda kwenda uwanjani na kizazi chenye kununua bidhaa halisi za klabu..