Mbali na Klabu ya Simba SC kuipongeza Young Africans, dakika chache baada ya kutwaa ubingwa wa 28 jana Jumatano (Juni 15) kwa kuifunga Coastal Union mabao 3-0, Meneja wa Habari na Mawasilino wa klabu hiyo ya Msimbazi Ahmed Ally ameibuka na jipya.
Young Africans imetwaa ubingwa wa Tanzania Bara kwa kufikisha alama 67, ambazo haziwezi kufikia na klabu yoyote inayoshiriki Ligi hiyo msimu huu 2021/22.
Ahmed Ally ametumia Kurasa zake za Mitandao ya Kijamii kuandika ujumbe ambao unaashiria jambo kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu, japo msimu huu haujafikia kikomo kwa michezo minne kusalia kwa klabu hiyo ya Msimbazi.
Ahmed amekiri kuwa, kikosi cha Simba SC msimu huu kilionyesha udhaifu, hali ambayo ilitoa nafasi kwa Young Africans kuwazidi kete na kufikia hatua ya kuongoza msimamo wa Ligi tangu walipopata nafasi hiyo baada ya michezo kadhaa kuchezwa hadi jana walipotangazwa ubingwa.
Ahmed Ally ameandika: Kukubali udhaifu wako ni njia bora ya kujipanga kwa wakati ujao
Kiroho saafi tumekubali yote yaliyotokea msimu huu na tumeanza mipango ya msimu ujao maana muda wa masononeko haupo na maisha yanatakiwa kuendelea
Tumebakiwa na mechi tano sisi kwetu hizi ni mechi za kumwagilia moyo
Mechi yetu ya leo dhidi ya Mbeya City ni mechi ya kumwagilia moyo tukutane kwa Mkapa saa 1:00 Usiku
Tunakutana kwa Mkapa tunafurahia tunajipongeza wakati mechi inaendelea tunamwagili moyo
Mpira ni burudani na burudani haihitaji makasiriko