Klabu ya Simba SC imesema wachezaji wake, Shomari Kapobe na Mohamed Hussein Zimbwe Jr bado wako katika ubora wao na hawajachoka kama baadhi ya wadau soka nchini wanavyoeleza, imefahamika.
Simba SC imelazimika kutoa ufafanuzi huo kufuatia hoja iliyochangiwa kocha na mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ambaye alisema mabeki hao wamechoka nani muda sahihi kwa David Kameta Duchu’ na Israel Mwenda kupewa nafasi.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema wachezaji hao wamecheza kwa muda mrefu hivyo inaonekana mashabiki wamewachoka na si kweli wameshuka viwango.
“Watu wamewachoka Kapombe na Tshalbalala (Zimbwe Jr), sasa wanawasingizia wamechoka, hoja hii imeshamiri baada ya mechi ya Power Dynamos.
“Kuna wakati watu walimchoka, Juma Kaseja na kila siku, akawa anaulizwa unastaafu lini, sio kwa sababu alishuka kiwango lakini walichoka kumuona, nchi hii Kapombe na Tshabalala bado wana muda zaidi wa kucheza kulingana na ubora wao, hivyo ni jukumu letu Wanasimba kuwalinda vijana hawa ambao ni tunu ya taifa,” amesema Ahmed.
Ameongeza timu nyingine hapa nchini zimehangaika kupata mabeki wa kulia na kushoto, lakini kwa muda mrefu klabu yao imekaa salama kwenye maeneo hayo.
“Tunao vijana wengine katika maeneo hayo (Duchu na Mwenda), ambao taratibu watarithi mikoba hiyo kwa wakati husika, lakini tukitaka kuwarithisha kwa presha tutaambulia presha,” ameongeza.