Meneja wa Habari na Mawasilino wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Ahmed Ally, ameingilia kati mjadala wa pendekezo la kununuliwa kwa mfumo wa ‘VAR’, ambao uliibuliwa mwishoni mwa juma lililopita na Waziri wa Fedha na Mipango Mwigulu Nchemba.
Waziri Mwiguli aliibua hoja hiyo, kufuatia YoungA fricans kukabiliwa na changamoto ya maamuzi yenye utata wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City FC, uliomalizika kwa sare ya 0-0.
Alisema atakaa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohammed Mchengerwa ili waongee uwezekano wa kutenga bajeti ya kununua VAR na nyasi bandia kwa ajili ya viwanja 10.
Mwigulu alieleza hayo kupitia Ukurasa wake wa Instagram akitolea mfano wa nafasi aliyonyimwa mshambuliaji wa Young Africans Fiston Mayele kufunga goli dhidi ya Mbeya City mwamuzi wa pembeni akidai ameotea.
Ahmed Ally ameingilia mjadala huo kwa kuweka andiko binafsi kwenye ukurasa wake wa Instagram, ambapo ameandika: Nimeona mjadala wa VAR ni wazo zuri naamini nia ni kuufanya mpira wa nchi hii uendelee kuwa bora zaidi.
Lakini kwangu VAR sio tatizo la msingi la mpira wetu, tatizo la msingi la mpira wetu ni sehemu ya kuchezea ( PITCH).
Tuna pitch mbovu sana nchi hii ukitoa Taifa, Azam Complex na Kaitaba, viwanja vingi vilivyosalia ni changamoto.
Mpaka leo viwanja vyetu vinapakwa chokaa kabla ya mechi na baada ya muda chokaa inafutika uwanja unakua hauna mistari, Mvua zikinyesha kidogo tuu mpira hauchezeki.
Mechi nyingi zinachezwa kwa kulazimishwa mfano mechi ya Mbeya City Vs Ruvu Shooting haikupaswa kuchezwa pale Sokoine.
Ushauri wangu kabla ya kuinvest kwenye VAR tungejikita kuboresha viwanja.
Europe walianza kuboresha viwanja ndo wakaja kwenye VAR.
Na kabla ya kufika kwenye VAR mamlaka husika waendelee kuboresha viwango vya waamuzi wetu wapate seminar za kutosha na wapate mechi kubwa za Afrika ili kuongeza uzoefu na kujiamini kwao.
Tukishamaliza kuwekeza kwenye Pitch ndo tutakuja kwenye VAR.