Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema msimamo wa Ligi Kuu kwa sasa umesababisha mji kuwa kimya licha ya watani zao wa jadi kuendelea kuongoza Ligi kwa tofauti ya alama 5.
Young Africans walilazimishwa sare ya bila kufungana dhidi ya Mbeya City Juzi Jumamosi (Februari 05), huku Simba SC ikiichapa Mbeya Kwanza FC jana Jumapili (Februari 06) bao moja kwa sifuri.
Ahmed amesema aliwahi kusema hadharani kuwa wapinzani wao wanapaswa kuwa watulivu kwa sababu Ligi bado mbichi, lakini cha kushangaza ujumbe wake haukuwafikia walengwa na badala yake waliendelea kutamba.
“Niliwahi kusema hapa, ligi bado sana na mapema mno kwa mtu kuanza kujisifia kuwa ndio bingwa, lakini kauli yangu ilichukuliwa kimzaha na leo watu wapo kimya,”
“Inapaswa watu kujitafakari sana, wafahamu kubwa msimamo wa ligi unabadilika kutokana na matokeo ya mpira ambayo hayana uhakika siku zote, walipaswa kusubiri angalau michezo 27 au 28, lakini mzunguuko wa kwanza haujaisha wanaanza kupiga kelele za ubingwa.” Amesema Ahmed Ally.
Kwa matokeo ya michezo ya Jumamosi na Jumapili, Young Africans imefikisha alama 36 ambazo zinaendelea kuwaweka kileleni, huku Simba SC ikishika nafasi ya pili kwa kuwa na alama 31.
Simba SC imekamilisha michezo yote ya mzunguuko wa kwanza na sasa inaanza maandalizi ya Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, huku Young Africans ikisaliwa na mchezo mmoja dhidi ya Mtibwa Sugar ili kukamilisha michezo ya mzunguuko wa kwanza.