Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally ameendelea kuwasihi Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo kuendelea kuwa na timu yao, licha ya kuwa kwenye wakati mgumu kwa sasa.
Jana Jumatano (Januari 26), Simba SC ilipoteza mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar kwa kufungwa bao 1-0, hali ambayo imeifanya klabu hiyo kuwa na tofauti ya alama 10 dhidi ya vinara wa msimamo wa Ligi Kuu Young Africans.
Ahmed Ally ametoa nasaha hizo kwa Mashabiki na Wanachama wa Simba SC kupitia ukurasa wake wa Instagram ambapo ameandika: Kuna wakati timu bora sana huwa inapoteza mchezo.
Jana tulikua kwenye ubora wetu wa hali ya juu, tulitawala sehemu yote ya mchezo.
Takwimu zinaeleza wazi kile ambacho tumekifanya Kaitaba, ni goli tuu la Kagera Sugar ndilo ambalo limefifisha ubora wetu.
Bado tupo kwenye ubora wetu, vipo vitu vichache vya kurekebisha naamini vitafanyiwa kazi kwa haraka.
Poleni sana ndugu zangu wa @simbasctanzania ni kipindi cha mpito.
Sisi tunajivunia ninyi tunafahamu tumepitia mengi kwenye ushabiki wetu ambao umetufanya tukomae na tuwe mashabiki bora Nchini.
Niwaombe msitoke kwenye reli mapambano bado yanaendelea…
Waache wacheke sasa ila atakaecheka mwisho ndo atacheka zaidi.