Kufuatia Malalamiko ya baadhi ya Mashabiki na Wanachama wa Simba SC kuhusu uwezo wa Kocha Msaidizi Seleman Matola, Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba Ahmed Ally ametoa tamko.
Wakati na baada ya mchezo wa Simba SC na KMC FC uliochezwa jana Jumatano (Septemba 07) Uwanja wa Benjamin Mkapa, baadhi ya Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo ya Msimbazi walipaza sauti zao kwa kuwataka viongozi kumuondoa Matola kwa kigezo cha kukosa mbinu, kama ilivyo kwa makocha walioondoka klabuni hapo.
Ahmed Ally amechukua jukumu la kujibu hoja za Mashabiki na Wanachama hao akionesha namna alivyopokea malalamiko yao.
Pia Ahmed Ally amewahimiza Mashabiki na Wanachama wa Simba SC kuwa watulivu na kutambua sababu za kiufundi ambazo wakati mwingine zinaweza kuifanya timu kuzidiwa kimbinu.
Ahmed Ally amesema: “(Wana-Simba) ni haki yao kusema hawamtaki yeyote ndani ya Simba. Leo watasema hawamtaki Matola kesho watasema hawamtaki Ahmed Ally.
“Unapopata matokeo mabaya Kubali vilio vya aina yoyote ile. Usiwapangie watu wazomee au walie Kwa kilio Cha namna gani”
“Nimesikia vilio vya Wana-Simba wao Kwa tathimini yao wanaona Matola ndio tatizo ndani ya Simba ila nimwambie tu tuko sawa sawa. Leo (Jana) tulizidiwa kimbinu na KMC na hata angekuwa Kocha gani bado matokeo tungeyapata hivihivi”
“Hoja yao ya kwamba wameondoka Makocha wengi halafu Yeye kabaki haina maana yoyote. Kama mtu anatimiza Majukumu yake kwanini umuondoe Kwenye Majukumu yake.”