Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba SC Ahmed Ally, ameendelea kuwasili Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho wameshindwa kufikia lengo la kutetea mataji ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’.
Simba SC ilizimwa na kupoteza kila kitu Jumamosi (Mei 28) baada ya kuambulia patupu katika mchezo wa Nusu Fainali Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ kwa kufungwa 1-0 na Young Africans jijini Mwanza kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.
Ahmed Ally amesema Uongozi wa Simba SC unafahamu Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo wameumizwa na kilichotokea msimu huu, kutokana na mategemeo makubwa waliokuwa nayo hapo awali, lakini hawana budi kukubaliana na ukweli wa mambo.
Amesema Uongozi wa Simba SC ulijipanga kutetea mataji yote msimu huu, lakini kilichotokea ni mipango ya Mungu, kwani hakutaka furaha yao iendelee msimu huu.
“Ninafahamu namna gani mashabiki wetu wameumia na ninajua machungu wanayoyapitia hivi sasa kwa sababu walikuwa na mategemeo makubwa, tumepoteza mchezo ambao tuliutegemea sana na ungetusaidia kufikisha nusu ya malengo yetu msimu huu”
“Kama utawala tulijitahidi kuhakikisha tunatwaa mataji ila mambo hayakuwa hivyo. Niwaambie tu msimu rasmi tumeumaliza na tunakamilisha tu ratiba kwenye ligi kuu lakini kiuhalisia msimu huu tunamaliza patupu bila ya taji lolote na ndo kitu kinachotuumiza wanasimba hatujazoea kumaliza msimu bila ya taji, inauma sana” Amesema Ahmed Ally
Simba SC ilijitengenezea ufalme wa Soka la Bongo kwa misimu minne mfululizo, huku ikitwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ mara mbili mfululizo, Ngao ya Jamii mara tatu Mfululizo na kufika Robo Fainali ya michuano ya Afrika mara tatu ndani ya miaka mitano.