Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema kuwa mshambuliaji wao kutoka DR Congo, Jean Baleke amewaahidi kufunga katika mchezo wao dhidi Young Africans.

Young Africans itakuwa mgeni wa Simba SC Jumapili (April 16) katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Ahmed Ally amesema “Tumeongea na mchezaji ambaye ni mshambuliaji wetu Jean Baleke mara baada ya kufanikiwa kufunga mabao mawili kwenye mchezo uliopita dhidi ya Ihefu na mwenyewe ametuahidi kuwa atafunga mabao katika mchezo dhidi ya Young Africans.”

Baleke katika michezo miwili iliyopita amefanikiwa kuifungia Simba SC mabao matano na yote dhidi ya Ihefu, jambo ambalo linawapa mzuka mashabiki wa klabu hiyo kuelekea mchezo dhidi ya mtani wao Young Africans.

Mara ya mwisho wababe hao kutoka Kariakoo jijini Dar walitoka sare ya bao 1-1 ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara Mzunguuko wa kwanza msimu huu 2022/23.

Carragher amkingia kifua Virgil van Dijk
Serikali kuajiri Wataalamu wa Afya 12,000: Dkt. Mollel