Wakati ikitambulisha rasmi jezi yake mpya itakayotumika katika msimu wa 2023/2024, mabosi wa timu hiyo wamesema hawajakurupuka katika mchakato wa usajili na kila mchezaji waliyemnasa, basi uamuzi wake umetokana na malengo maalumu.

Juzi Alhamis (Julai 20) Simba SC ilitangaza kuwanasa wachezaji wapya watatu, wote raia wa Tanzania ambao ni straika, Shabani Chilunda, beki wa kati, Hussein Kazi na kiungo mkabaji, Abdallah Hamisi, ambaye amewahi kucheza soka la kulipwa Kenya.

Meneja Habari wa Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema hawajakurupuka kuwasajili wachezaji hao, bali wamefanyika mchakato mkubwa kwa kufuata mapendekezo ya benchi la ufundi ili nyota hao na wengine wawe msaada katika kikosi chao.

“Tuna michuano mingi sana safari hii, Ngao ya Jamii, Super League, Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la Mapinduzi, Kombe la FA, Ligi ya Mabingwa Afrika na mingine itakayojitokeza, lazima tuwe na kikosi kipana kwa ajili ya kufanya mabadiliko ya mara kwa mara, badala ya kuchezesha wachezaji wale wale,” amesema Ahmed.

Aliongeza usajili huo ni matekelezo ya Kocha Mkuu Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ambaye aliagiza kuelekea msimu ujao anataka kila namba iwe na wachezaji wawili au watatu wenye uwezo unaofanana au kukar- ibiana.

Chilunda, Mshambuliaji wa zamani wa Azam FC amesajiliwa kwa mkataba wa miaka miwili akiwa mchezaji huru, akiwa amewahi kuzichezea klabu za CD Tenerife na CD Izarra zote za Hispania na Moghreb Tetouan ya Morocco.

Nyota huyo anatarajia kwenda kuwania namba dhidi ya John Bocco, Jean Baleke na Mzambia Moses Phiri.

Kazi, aliyetokea Geita Gold na kuwahi kuzichezea klabu za Mbeya Kwanza, Polisi Tanzania na soka la kulipwa, Shelisheli, anakwenda kupambania namba dhidi ya Henock Inonga, Kennedy Juma na Che Fondoh Malone, huku Hamisi, Mtanzania ambaye amecheza soka la kulipwa nje ya nchi kwa muda mrefu kwenye klabu za Muhoroni Youth FC, Sony Sugar, Bandari FC zote za Kenya atachuana dhidi ya Mzamiru Yassin, Sadio Kanoute, Fabrice Ngoma na Nassoro Kapama.

Kikosi cha Wekundu wa Msimbazi kwa sasa kiko Uturuki kikifanya maandalizi ya msimu mpya na kitarejea nyumbani tayari kwa utambulisho wa katika Tamasha la Simba Day 2023 litakalofanyika Agosti 6, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Meshack Abraham anaswa Dodoma Jiji FC
PICHA: Siku ya Mwananchi yafunika Dar