Meneja wa Habari na Mawasilino wa Klabu ya Simba SC Ahmed Ally ametamba kikosi chao kitaendelea kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa, baada ya kuanza vyema hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast.
Simba SC iliibuka na ushindi wa 3-1 dhidi ya Mabingwa hao wa Ivory Coast, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, jana Jumapili (Februari 13).
Ahmed Ally ametoa tambo hizo alipozungumza na Dar24 Media, ambapo amesema kikosi cha Simba SC kilijiandaa kushinda mchezo huo ambao ulikua muhimu sana kwao kwa lengo la kuhakikisha wanaendeleza rekodi ya kushinda nyumbani.
“Tulijiandaa kushinda mchezo huu, tunamshukuru Mungu tumekamilisha hili, huu ni mwanzo tu, mengine mengi mazuri yanakuja.”
“Simba hiii ndio ya kimataifa na tumethibitisha kwa kuifunga timu yenye hadhi ya kimataifa, ushindi wa 3-1 ni heshima kubwa kwetu kama Simba SC na kwa taifa kwa ujumla.”
“Tutahakikisha tunashinda katika michezo yote tutakayocheza hapo na ikiwezekana hata katika viwanja vya ugenini tutashinda pia, niliwahi kusema hili wakati tunajiandaa na mchezo huu lakini watu wengi walipuuzia wakidhani nilikua nafanya mzaha, lakini ukweli umejidhihirisha uwanjani na nyinyi mmeona.” Amesema Ahmed
Wakati Simba SC ikiaanza kwa ushindi wa 3-1, RS Berkane ya Morocco nayo imeanza kwa kuibamiza US Gendamarie ya Niger kwa mabao 5-3, hivyo kulifanya Kundi D kuwa na timu mbili zenye alama 3.