Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally ameguswa na kauli iliyotolewa jana Jumatatu (Oktoba 03) na Afisa Habari wa Young Africans Ally Kamwe kuhusu uhamasishaji wa Mashabiki kuelekea mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Al Hilal ya Sudan.
Young Africans itakuwa mwenyeji wa mchezo wa Mkondo wa Kwanza dhidi ya Al Hilal ya Sudan Jumamosi (Oktoba 08), Uwanja wa Benjamin Mkapa, kabla ya kwenda Khatoum-Sudan kwa mchezo wa Mkondo wa Pili utakaopigwa kati ya Oktoba 14-16.
Ally Kamwe alisema katika shughuli atakazozifanya juma hili kuelekea mchezo wa Mkondo wa Kwanza kwa ajili ya kuhamasisha Mashabiki kufika Uwanja wa Banjamin Mkapa kuishangilia timu yao, hatotumia ‘KISPIKA’ mitaani, na kama atafanya hivyo yupo tayari kuchapwa Bakora.
“Kutembea na Kispika mtaani ili kuhamasisha Mashabiki Ni sawa na mtu mwenye njaa anasubiri apigiwe kelele akale wakati chakula anakiona, mkiniona ninafanya hivyo mnichape Bakora.” alisema Ally Kamwe
Ahmed Ally ametumia kurasa zake za Mitandao ya kijamii kujibu kauli hiyo ya Ally Kamwe, kwa kusisitiza ataendelea kufanya hivyo kama sehemu ya kazi yake aliyoianza tangu alipotangazwa kuwa Meneja wa Habari na Mawasilino Simba SC.
Amendika kabla ya mchezo wa Mkondo wa Pili wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Primira de Agosto ya Angola utakaopigwa Dar es salaam Jumapili (Oktoba 16), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, atafanya hivyo kama kawaida.
Ahmed ameandika: “Alianza Ashura cheupe kuumia na Kispika, Sasa wajukuu wa Ashura cheupe wanaumia na Kispika.”
“Niite Mwambaa Kispika, Ukisikia wanabweka jua imewaingia, Kispika kitaingia tena mtaani kwenye mechi ya marudiano ya De Agosto.”
“Hatuachi na hatujamalizaaaaa”