Meneja wa Habari na Mawasilino wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Ahmed Ally amejibu hoja za klabu ya Young Africans kuhusu waamuzi wa Ligi Kuu.
Young Africans kupitia Idara ya Habari na Mawasilino ilizungumza na Waandishi wa Habari jana Jumanne (Februari 08) na kueleza namna wanavyosikitishwa na baadhi ya waamuzi wanaochezea Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2021/22.
Ahmed Ally amejibu hoja hiyo alipohojiwa na Radio Free Africa leo Jumatano (Februari 09), ambapo amesema katika maelezo yaliyotolewa na Young Africans kwao hayana tija yoyote, zaidi ya kuamini wahusika wanatapatapa kwa kujificha kwenye kivuli cha Waamuzi.
Amesema kuihusisha Simba SC katika hoja hiyo wamekosea sana, kwani haijawahi kutokea kwa kiongozi yoyote kuhusika na sheria 17 za mchezo wowote unaowahusu ama kuihusu Young Africans.
“Hujawahi kuona Barbara anatoa kadi nyekundu, hujawahi kumuona Try Again akiongeza dakika hujawahi kumuona Murtaza Mangungu anatoa kadi nyekundu uwanjani wala hujawahi kuniona mimi nikiongeza dakika, hivyo haya malalamiko ya waamuzi hayatuhusu, lakini walitolewa ligi ya mabingwa mapema sana vipi na huko shida ilikuwa ni waamuzi?” amesema Ahmed Ally
Simba SC na Young Africans zinaendelea kupambana kwenye mbio za Ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu 2021/22, huku Mabingwa watetezi wakishika nafasi ya pili kwenye msimamo wakiachwa kwa alama 6.
Young Africans inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufikisha alama 36, huku ikicheza michezo 14, ilihali Simba SC ikiwa imecheza michezo 15 na kufikisha alama 31.