Baada ya kutwaa Ubingwa wa Kombe la Mapinduzi 2022 kwa kuifunga Azam FC bao 1-0 jana Alhamis (Januari 13), Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba SC Ahmed Ally amewatumia salamu Mbeya City kwa kuwaambia wajipange.
Simba SC ilinyakua taji la Mapinduzi 2022, Uwanja wa Aman kisiwani Unguja-Zanzibar, kwa bao la Penati iliyofungwa na Mshambuliaji kutoka nchini Rwanda Meddie Kagere, baada ya Mlinda Lango wa Azam FC Mathias Kigonya kumchezea hovyo Pappe Ousman Sakho.
Ahmed amesema baada ya kukamilisha shughuli ya Mapinduzi 2022, nguvu zao wanazielekeza Ligi Kuu Tanzania Bara ambapo watacheza dhidi ya Mbeya City Jumatatu (Januari 17), katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine Jijini Mbeya.
“Tumemaliza Mapinduzi Cup hapa Zanzibar, timu inarejea Dar es salaam, kisha itasafiri kuelekea Mbeya kwa ajili ya mchezo wetu na Mbeya City, nawatumia salamu hawa jamaa nao wajipange maana hatutaki mzaha kabisa mwaka huu 2022.”
“Lengo letu ni kucheza kwa malengo ili mwishoni mwa msimu tutimize tulichokisudia, tumefanikiwa hapa Zanzibar kwa kutwaa Kombe la Mapinduzi, sasa tunaendelea kusaka mataji mengine.”
Simba SC inarejea kwenye Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa nafasi ya Pili katika Msimamo wa Ligi hiyo kwa kumiliki alama 24 ilizozipata kwenye michezo 10, ikitanguliwa na Young Africans yenye alama 29 baada ya kucheza michezo 11.