Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC Ahmed Ally amefurahishwa na mabadiliko ya muda mfupi ya kikosi chao ikiwa ni siku chache tangu Kocha Mkuu Abdehak Benchikha akabidhiwe timu.
Kocha huyo kutoka nchini Algeria mara baada ya kutangazwa kuinoa timu hiyo, aliahidi makubwa msimu huu ikiwemo kuipa makombe yote wanayoshindania sambamba na burudani ya soka safi.
Ahmed Ally amesema kuwa kocha wao Benchikha anastahili pongezi nyingi, ni baada ya kukifanyia mabadiliko kikosi, ambacho ndani ya siku chache fitinesi za wachezaji imeongezeka.
Amesema kuwa ufundi, hali ya kujiamini na morali imeongezeka, hiyo itawafanya wachezaji wao wapambane katika michezo yao inayofuatia Ligi Kuu Tanzania bara michuano ya Kimataifa.
Ameongeza kuwa, anataka kuona kiwango hicho cha kila mchezaji kikiendelea kuongezeka, ili kufikia malengo ya msimu huu kuwapoka Young Africans mataji waliyoyachukua katika misimu miwili ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.
“Benchikha amethibitisha ubora wake ndani ya siku chache ambazo, tumemkabidhi jukumu la kuifundisha timu yetu, amefanikiwa kufanya mabadiliko makubwa katika timu.
“Simba SC iliyocheza mchezo dhidi ya Wydad Casablanca, ndiyo Simba tunayoijua sisi inapiga pasi na kutawala mchezo, licha ya matokeo mabaya tuliyoyapata ya kufungwa bao 1-0.
“Ninasubiria Simba SC iliyo bora na imara itakayobeba mataji yote ya ndani na kufika mbali kimataifa, chini ya kocha mwenye CV kubwa Afrika,” amesema Ahmed Ally