Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC Ahmed Ally amesema bado ana matumaini na Kikosi cha Klabu hiyo kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu 2022/23.

Simba SC imepoteza michezo miwili ya kwanza ya Kundi C, kwa kufungwa 1-0 dhidi ya Horoya AC ugenini (Guinea) kisha ikapoteza nyumbani Dar es salaam dhidi ya Raja Casablanca ya Morocco.

Ahmed Ally amesema bado Kikosi chao kina nafasi kubwa ya kusonga mbele, licha ya kuachwa kwa tofauti ya alama 06 dhidi ya vinara wa Kundi C Raja Casablanca, wakifuatiwa na Horoya AC wenye alama 04 na Vipers SC wakiwa na alama 01.

Ahmed Amesema Simba SC imebakiza michezo minne ya Kundi C, ambayo inatoa nafasi kwa kikosi chao kufanya lolote na kumaliza katika nafasi mbili za juu kwenye kundi hilo.

Amesema atakuwa mtu wa mwisho kuamini kama Simba SC imeshindwa kufuzu hatua ya Robo Fainali ya Michuano hiyo msimu huu, licha ya kuamini wanakabiliwa na Ratiba ngumu.

“Bado tuna michezo mingine minne, nitakuwa mtu wa mwisho kuamini Simba SC hatuendi Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika, Ratiba yetu ni ngumu, lakini tutafuzu, naomba nisisitize nitakuwa mtu wa mwisho kuamini Simba SC haiendi Robo Fainali” amesema Ahmed Ally

Simba SC mwishoni mwa juma hili itaendelea na Mchaka Mchaka wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa kucheza na Mabingwa wa Uganda Vipers SC, mjini Entebe-Uganda katika Uwanja wa St Merry’s.

Kabla ya kuelekea Uganda Simba SC itacheza mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC kesho Jumanne (Februari 21), katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Kwa sasa Simba SC ipo nafasi ya pili katika Msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 53, ikitanguliwa na Mabingwa watetezi Young Africans yenye alama 59.

Young Africans warejesha shukurani
Azam FC, Young Africans zaivuruga KMC FC