Meneja Habari na Mawasilino Simba SC Ahmed Ally amewapa pole Mashabiki na Wanachama wa Klabu hiyo, kufuatia matokeo ya 1-1 dhidi ya Kegara Sugar.
Simba SC ilicheza ugenini jana Jumatano (Desemba 21) majira ya Usiku Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba-Kagera, huku ikitangulia kufungwa bao la mapema na wenyeji wao kupitia kwa Deus Bukenya dakika ya 15, kabla ya Simba SC kusawazisha kwa bao la kichwa lililofungwa na Beki kutoka DR Congo Enock Inonga Baka dakika ya 39 Kipindi cha Kwanza.
Ahmed Ally ametumia Kurasa zake za Mitandao ya kijamii kutoa pole hizo kwa Mashabiki na Wanachama, huku akisisitiza mapambano bado yanaendelea ili kufikia malengo waliojiwekea msimu huu 2022/23.
Ahmed ameandika: Pamoja na juhudi zote ambazo wachezaji wetu wamezifanya na kujitoa kwa nguvu na maarifa yote lakini furaha haijaja upande wetu.
Mpinzani amekua bora na hatimae tumevuna alama moja
Si nzuri kwetu kulingana na malengo yetu lakini hatuna budi kuipokea na kusonga mbele bado tuna mechi nyingi.
Poleni sana ? tuendeleeni na mapambano.
Kwa matokeo hayo Simba SC imefikisha alama 38 zinazoiweka nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikitanguliwa na Young Africans iliyo kileleni kwa kuwa na alama 44, huku Azam FC ikiwa nafasi ya tatu kwa kufikisha alama 37.
Simba SC itarejea tena Uwanjani mwishoni mwa juma hili jijini Mwanza kwa kucheza dhidi ya KMC FC, itakayoutumia Uwanja wa CCM Kirumba kama Uwanja wake wa nyumbani.