Meneja wa Habari na Mawasilino wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Ahmed Ally amesema hakupata wakati mgumu kukubali kujiunga na klabu hiyo, baada ya kuombwa na Uongozi.
Ahmed Ally alitangazwa kuwa Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC mwanzoni mwa mwezi Januari 2022, akichukua nafasi Haji Manara aliyeondoka klabuni hapo mwishoni mwa msimu uliopita.
Akizungumza na Clouds FM kupitia kipindi cha Sports Extra Ahmed Ally amesema ilikua rahisi kwake kukubali kuajiriwa Simba SC kutokana na mazingira ya kuondoka kwa aliyemtangulia (Haji Manara), klabuni hapo.
“Aliyeondoka (Haji Manara) hakuondoka vizuri, hivyo kwangu haikuwa taabu sana kuvaa viatu vyake machoni mwa WanaSimba.”
“Aliyewaachia mashabiki ‘maumivu moyoni’, hivyo tafsiri yake ni kwamba mimi nilienda sehemu ambayo watu hawamkumbuki aliyeondoka, hivyo sikuwa nafeel any pressure.” amesema Ahmed Ally.
Baada ya Haji Manara kuondoka Simba SC, Ezekiel Kamwaga alikaimu nafasi ya Mkuu Idara ya Habari na Mawasilino ya klabu hiyo, ambayo aliwahi kuitumikia kama Afisa Habari na Katibu Mkuu miaka ya nyuma.