Mabingwa wa Soka Tanzania Bara na Wawakilishi wa Afrika Mashariki na Kati kwenye michuano ya Kimataifa Simba SC, wapo kwenye maandalizi makali ya kuikabili RS Berakene ya Morocco.
Simba SC itakua mwenyeji wa mchezo huo wa Mzunguuko wa 04 wa Kundi D, Kombe la Shirikisho utakaopigwa Jumapili (Machi 13), Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es salaam, huku ikiwa na deni la kulipa kisasi cha kufungwa mabao 2-0, kwenye mchezo wa Mzunguuko wa 03 wa Kundi D, uliounguruma mjini Berkane-Morocco Februari 27.
Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amezungumza na WASAFI MEDIA mapema leo Jumatano (Macho 09), ambapo amesema kikosi chao kipo katika maandalizi makali ya mchezo huo ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na kila shabiki wa soka Tanzania na Afrika Mashariki na Kati.
Ahmed amesema wanatambua wana deni kubwa la kusaka ushindi katika mchezo huo ili kujiweka katika mazingira mazuri kwenye msimamo wa Kundi D, hivyo kila mmoja ndani ya klabu anapambana kwa nafasi yake ili kufanikisha azma na malengo waliojiwekea kuelekea Jumapili (Machi 13).
“Tuna wachezaji wanaofahamu nini cha kufanya katika michezo kama hii, wanajua wanajiandaa na mchezo wa aina gani, hivyo kocha na wasaidizi wake wanapanga mbinu ambazo zitafanikisha lengo la kufanya vizuri nyumbani.”
“Ukiangalia Kundi D, limetengeneza kasumba ya kila mmoja ashinde nyumbani kwao, mpaka sasa kila mmoja amepambana kwake na kupata matokeo isipokua USGN alipocheza na sisi pale kwao Niger ndio aliambulia matokeo ya sare, lakini wengine wote wamepata matokeo katika viwanja vyao vya nyumbani, hivyo hata sisi tunataka kuthibitisha hilo kwa Mkapa siku ya Jumapili (Machi 13).”
“Hivyo wachezaji wanafahamu jukumu lao katika mchezo wetu dhidi ya RS Berkane, wanajua hakuna mahala pengine pa kupata alama tatu zaidi ya Uwanja wa nyumbani kama ilivyo desturi ya kundi hili, kwa hiyo ni mchezo wetu ambao ni lazima tushinde, na uzito wake ni kwamba kila mmoja wetu ndani ya Simba SC anafahamu nini cha kufanya.” amesema Ahmed Ally
Hadi sasa Msimamo wa Kundi D, unaonyesha kuwa RS Berkane inaongoza ikiwa na alama 06, ikifuatiwa na Simba SC yenye alama o4 sawa na USGN ya Niger huku ASEC Mimosas ya Ivory Coast ikiburuza mkia ikiwa na alama 03.