Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally amesema kikosi chao kipo katika maandalizi ya mwisho kabla ya kuanza safari ya kuelekea Marrakech nchini Morocco, kwa ajili ya mchezo wa Mzunguuko watatu wa Kundi B, dhidi ya Wydad Casablanca.
Kikosi cha Simba SC jana Jumatatu (Desemba 04) kilirejea kambini kujiandaa na mchezo huo ambao utatoa taswira ya safari yao ya kutinga Robo Fainali, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kupitia Kundi B.
Ahmed Ally amesema amesema baada ya kurejea kambini, kikosi chao kilianza mazoezi jana saa tisa, kwa ajili ya mchezo dhidi ya Wydad Casablanca unayotarajiwa kucheza Jumamosi (Desemba 09) kwenye Uwanja wa Marrakech nchini Morocco.
“Tuliporejea tuliwapa mapumziko kidogo wachezaji wetu, lakini walirejea jana, saa tisa na kuanza rasmi mazoezi na kambi kwa ajili ya mechi ya tatu dhidi ya Wydad, ni mechi ngumu kwa sababu jamaa wamepoteza zote mbili za mwanzo, hivyo watataka kuamkia kwetu, lakini na sisi tunajipanga, kwa siku hizi kadhaa nadhani kocha wetu atapandikiza ujuzi na ufundi wake kwa wachezaji.
“Tumeona siku chache tu baada ya kuichukua timu kuna kitu kimeanza kuonekana, nadhani baada ya muda kidogo timu itakuwa sawa, umeona wachezaji wanajituma, wanakimbia, na hata utimamu wa mwili umeanza kuongezeka,” amesema Ahmed Ally.
Asec Mimosas ya Ivory Coast inaongoza msimamo wa Kundi B, ikiwa na pointi nne na mabao mawili, sawa na Jwaneng Galaxy inayoshika nafasi ya pili, lakini yenyewe ina bao moja, Simba SC ikiwa namba tatu kwa pointi mbili na Wydad ikiburuza mkia bila pointi.