Baada ya kuondolewa na Al Ahly ya nchini Misri katika michuano ya African Football League (AFL), Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally amesema akili zao wanazielekeza katika Ligi Kuu Tanzania Bara na kikubwa kurejea kileleni.
Kauli hiyo huenda ikawa kijembe kwa wapinzani wao, Young Africans ambao wanaongoza ligi wakiwa na pointi 15 sawa na Simba SC ambao wapo nyuma mchezo mmoja.
Simba SC wanatarajiwa kujitupa kwenye Uwanja wa Mkapa Jijini Dar es salaam kesho Jumamosi (Oktoba 28) kuvaana dhidi ya Ihefu FC katika mchezo wa ligi.
Ahmed amesema kuwa hasira zote za kuondolewa katika African Footabll League, wanazihamishia katika ligi kwa lengo la kubeba ubingwa huo.
Ahmed ameongeza kuwa kwa kuanza wataanza na mchezo ujao wa ligi dhidi ya Ihefu, ambao wamepanga kuwashushia kipigo kizito kwa lengo la kuwaondoa kileleni Young Africans.
Ameongeza kuwa wapinzani wao Young Africans wamekaa kwa muda katika nafasi hiyo, wakati wao wakiwa wanacheza michuano hiyo mipya ya AFL.
“Rasmi tumerejea katika ligi, kwa kuanza tunatarajiwa kuanza na Ihefu FC kesho Jumamosi tutakapokutana kwenye Uwanja wa Mkapa katika mchezo wa ligi.
“Tumepanga kurejea kwa kishindo katika ligi, kwa kutoa dozi kwa kila timu tutakayokutana nayo, ninafahamu haitakuwa rahisi kupata ushindi huo, lakini wachezaji wetu watahakikisha wanapambana. Ihefu hawawezi kutusumbua, wapo wanaowasumbua lakini sio wao, tumepanga kuonyesha ukubwa wetu Simba SC katika ligi,” amesema Ahmed.