Mashabiki wa Simba SC wamepewa nafasi maalum na Uongozi wa klabu hiyo, baada ya kutwaa tuzo ya Mashabiki Bora wa Michuano ya African Football League 2023.
Simba SC ilitangazwa kuwa mshindi wa Tuzo hiyo mwishoni mwa juma lililopita wakati wa sherehe za kukabidhi Ubingwa wa AFL zilizofanyika Afrika Kusini, ambapo Mamelodi Sundowns ilitawazwa kuwa Mabingwa wa michuano hiyo kwa kuifunga Wydad AC ya Morocco.
Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema Tuzo hiyo kamwe haitakaa ofisini na badala yake itatembezwa kwenye matawi ya Simba SC nchi nzima, ili kuthibitisha mchango wa Mashabiki walioutoa.
“Tuzo ya Mashabiki Bora wa AFL 2023 haitakaa kwenye ofisi za Simba SC bali itakuwa inatembea kwenye matawi mbalimbali. Lakini pia tutakuwa na mfano ya Tuzo kama hii ambayo tutaipeleka sehemu mbalimbali ili wabaki na kumbukumbu.”
Katika hatua nyingine Ahmed Ally amewataka Mashabiki wa Simba SC kuhakikisha wanafika uwanjani kwa wingi Jumamosi (Novemba 25) kwa ajili ya kuishangilia timu yao itakapocheza dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast.
Amesema dhamira kuu ya Simba SC kuelekea mchezo huo ni kuihakikishia Dunia huwa hawabahatishi kuujaza Uwanja wa Benjamin Mkapa, hivyo ni wasaa wa kila shabiki kuhakikisha anafika Uwanjani hapo.
“Safari hii tunakwenda kuwashangaza watu, tutaujaza uwanja wa Mkapa. Niwambie Wanasimba kama una hasira uje nazo furaha utaikuta uwanjani.”
“Tiketi tunaanza kuuza leo, nunueni tiketi twendeni uwanjani. Ni kweli tulikuwa hatuchezi mpira wetu wa kuvutia lakini tunakwenda kubadilisha benchi la ufundi, tunategemea Simba itakayokuja kuwa na mabadiliko.”
“Kauli mbiu yetu ya mchezo dhidi ya ASEC Mimosas ni Twendeni Kinyama, Mashabiki Bomba.” amesema Ahmed Ally.