Kipigo cha 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting kimempa jeuri Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally, ambaye amekua mstari wa mbele kukisifia kikosi cha klabu hiyo kila kukicha.
Ruvu Shooting ilikua mwenyeji wa mchezo wa Hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho Tanzania Bara jana Jumatano (Februari 16), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam na kukubali kipigo hicho cha aibu, tangu msimu huu 2021/22 ulipoanza.
Ahmed Ally amesema ushindi huo mkubwa ni sehemu ya kurejesha heshima ya Simba SC iliyokua imepotea katika michezo ya ndani msimu huu, baada ya kupoteza dhidi ya Mbeya City na Kagera Sugar, huku wakitoa sare kwenye michezo minne ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Amesema timu nyingi za Tanzania zilitaka kuleta mazoea mabaya na Simba SC na kuamini timu hiyo imekua ya kawaida, hivyo iliwalazimu kusaka ushindi mzito ili kuonesha bado wana kikosi bora kinachoweza kupata ushindi mnono.
“Hii ni salamu kwa wengine ambao wametangulia katika Michezo ya Robo Fainali ya Michuano hii ya Kombe la Shirikisho, Sisi ndio mabingwa watetezi na tumedhihirisha hilo kwa kuwapiga Ruvu Shooting mabao 7-0”
“Naamini waliotangulia kwenye Hatua ya Robo Fainali roho zao zinawadunda huku wakiomba wasikutane na Simba SC ambayo ilionekana ya kawaida sana, nakiri wazi kwamba heshima yetu imeendelea kujidhihirisha na hatukuwahi kushuka katika hilo.” Amesema Ahmed Ally
Kwa matokeo hayo Simba SC imetinga hatua ya Robo Fainali ya Michuano ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ikiungana na Pamba FC, Young Africans, Coastal Union, Azam FC, Polisi Tanzania, Kagera Sugar na Geita Gold FC.