Meneja Habari na Mawasiliano wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Ahmed Ally amesema katika watu ambao hawampi hofu hata kidogo katika nchi hii ni klabu ya Young Africans.
Ahmed Ally ametoa kauli hiyo leo Jumatano (Febriari 02) alipohojiwa kwenye kipindi cha Luninga cha 10TVE kilichorushwa na Televisheni ya ETV.
Amesema Young Africans kukaa kwao kileleni hakumpi hofu hata kidogo, ila ingekuwa pale juu ipo timu kama Dodoma Jiji FC angeshtuka kwa kuwa ni Surprize kwa timu hiyo.
Ameongeza kuwa Young Africans imezoea kukaa hapo juu na kuzurura hapo na baadae kuporomoka na anaamini kikubwa msimu huu klabu hiyo ya Jwangani imeongeza tu ‘MAKELELE’ na sio Ubora wa kikosi.
“Kwangu sina wasiwasi kabisa na hawa jamaa kuongoza ligi kwanza hilo halinisumbi hata kidogo, wamekua wakishika nafasi hiyo na kuzurura hapo kisha wanashuka na sisi tunapanda na kutwaa ubingwa, yaani hili halinipi shida kabisa kabisa.” Amesema Ahmed Ally.
Ahmed Ally ametoa tambo hizo huku klabu ya Simba SC ikiachwa kwa alama 10 na Young Africans katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakicheza michezo 13 kila mmoja.
Simba SC ipo nafasi ya pili ikiwa na alama 25 huku Young Africans ikiwa kileleni kwa kufikisha alama 35.