Uongozi wa Simba SC, umesema kwamba, kupoteza kwa Young Africans katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ihefu FC, kuliwaongezea nguvu ya kupambana na kupata matokeo mazuri katika michezo miwili iliyopita ikiwa ni njia ya kubeba ubingwa.
Young Africans baada ya kupoteza dhidi ya Ihefu FC kwa mabao 2-1 kabla ya kushinda 3-0 dhidi ya Geita, Simba SC walishinda michezo miwili iliyofuatia dhidi ya Tanzania Prisons na Singida Fountain Gate.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmedy Ally, amesema kwa kiasi kikubwa muamko wa ushindi na kupambana ulipatikana baada ya Young Africans kupoteza mchezo dhidi ya Ihefu FC.
“Kusema ukweli baada ya Young Africans kupoteza mchezo wao kwa kiasi kikubwa tulipata muamko na hamasa kubwa ya kupambana na kuhakikisha tunashinda michezo yetu yote ili tuweze kukaa kileleni.
“Tunashukuru kwa kweli tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa, watu wameona ni kwa jinsi gani timu ilipambana na kweli matokeo yakapatikana, mpaka sasa unaona tunaongoza ligi.
“Nataka niwaambie Wanasimba kuwa malengo yetu msimu huu ni kuona tunafanikisha jambo letu la kutwaa ubingwa baada ya kuukosa ubingwa huu kwa misimu miwili,” amesema kiongozi huyo.