Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu kifungo cha mwaka mmoja jela au faini ya shilingi milioni 5, Elizabeth Asenga mwenye umri wa miaka 40 baada ya kumkuta na hatia ya kusambaza ujumbe wa kumkashfu Rais John Magufuli kupitia WhatsApp.

Akisoma hukumu hiyo leo, Hakimu Huruma Shaidi alisema kuwa baada ya kupitia ushahidi uliotolewa pamoja na utetezi wa Asenga ambaye ni mhasibu wa Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Joseph, Mahakama imejirisha pasipo shaka kuwa ana hatia.

Katika shtaka dhidi yake, Asenga anadaiwa kuwa Agosti 6 mwaka jana alituma ujumbe wa kumkashfu Rais Magufuli kwenye ‘group’ la WhatsApp la STJ Staff Social Group huku akijua kufanya hivyo ni kosa.

Ujumbe huo ulikuwa na maneno ya kashfa na ulitumwa mapema asubuhi na Asenga ambaye alionesha kutaka kuteka umakini wa watu wote kabla hajatoa ujumbe wake.

Hata hivyo, Asenga aliweza kulipia faini ya shilingi milioni tano na kuweza kukwepa adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja jela.

 

Roma asema kundi la ‘Rostam’ litavunjwa na michepuko
Nyumba ya mbunge Bobi Wine yashambuliwa kwa vilipuzi