Kamanda wa polisi Mkoa wa Kagera, Revocatus Malimi amesema wamemkamata Mrisho Ibrahimu mwenye umri wa miaka 34 kwa tuhuma za kukutwa na sare za Jeshi la Wananchi (JWTZ), ambazo aliziiba kutoka katika nyumba ya baba mkwe wake, mkoani Arusha.
Akieleza sababu ya kufika mkoani Kagera, Ibrahimu amesema, alimfuata mpenzi wake wa kando (mchepuko) ambaye alimpata kupitia mitandao ya kijamii na kuwa alipofika mkoani humo hakubahatika kukutana naye, ndipo alipoanza kufanya utapeli ili apate nauli ya kurudi alipotoka
Kamanda Malimi amesema kuwa kijana huyo alikamatwa akiwa katika nyumba moja ya kulala wageni, eneo la Kamachumu wilayani Muleba. Alisema baada ya kuhojiwa amekiri kuiba sare za baba mkwe wake, ambaye ni Askari wa JWTZ mkoani Iringa; na kujifanya ni Askari wa Jeshi hilo kikosi cha mizinga mkoani Arusha.
Kwa mujibu wa EATV, mtuhumiwa mwenyewe amekiri kuchukua sare hizo za jeshi ili asilipe nauli kwenye basi wakati wa safari yake.