Mwanaume mmoja Nchini Kenya ameiambia mahakama kuwa alipelekwa na ibilisi kwenye gari la polisi na kuiba simu za OCS.

Mohammed Noor ambaye ana umri wa miaka 47 alishtakiwa kwa kuiba simu mbili za OCS Adan Shukri jijini Nairobi, alifikishwa katika Mahakama ya Milimani jijini Nairobi anadaiwa kutenda kosa hilo mnamo Februari 27, 2022, katika kituo cha basi karibu na River Road Nairobi na alikiri mashtaka mbele ya Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Nairobi Bernard Ochoi na kuomba asamehewe.

“Unashtakiwa kuwa mnamo Februari 27, 2022, katika steji ya basi ya Tahmeed kando ya River Road, uliiba simu mbili za rununu za aina ya Tecno na Nokia zenye thamani ya KSh 30,000, mali ya Adan Shukri,” karatasi ya mashtaka ilisema.

Mohammed alikiri mashtaka mbele ya Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Nairobi Bernard Ochoi na kuomba asamehewe akisema ni shetani aliyemwambia aibe. “Mzee nakuomba msamaha. Ni Shetani aliyenipeleka kwa gari la polisi na kuniambia niibe simu hizo,” alisema mshtakiwa.

Aidha aliiambia mahakama kuwa ana mke ambaye amelazwa hospitalini baada ya kujifungua mtoto wao na kuiomba mahakama imsamehe akiahidi kutorudia kosa hilo.

OCS huyo ambaye aliibiwa simu anahudumu katika Kituo cha Polisi cha Suguta huko Mar Mar, kaunti ya Samburu, alikuwa Nairobi kwa shughuli rasmi za kikazi.

Kulingana na ripoti ya polisi, siku aliyokamatwa mtuhumiwa, maaskari kutoka kituo cha Central walikuwa kwenye doria ya kawaida walipokutana na mshukiwa ambaye alikuwa ameshikwa na wananchi na walimkamata na kukuta alikuwa na simu mbili za mkononi na kutaka maelezo kuhusu simu hizo na mmiliki alipigiwa simu na kikosi kilichokuwa kikifuatilia kesi hiyo.

“Alitafutwa na kuthibitisha kuwa simu yake ya kibinafsi na ile ya kazi ziliibiwa kwenye gari la polisi aina ya Land Cruiser katika steji ya Tahmeed alipokuwa akikata tikiti ya kwenda Kwale,” ripoti hiyo ilisema.

Wakili wa upande wa mashtaka James Gachoka aliomba mahakama iachilie simu hizo kwa OCS, ombi ambalo lilikubalika na mahakama na Hakimu aliamuru ripoti ya kabla ya hukumu iwasilishwe mahakamani kufikia Machi 4, 2022, kabla ya kumfunga jela mtuhumiwa.

Geita waidai TAMISEMI V8 yao ya Mil. 400
Mshindo Msolla awasihi Wachezaji, Kocha Young Africans