Mlinda Lango chaguo la kwanza Simba SC, Aishi Manula anaendelea vizuri na matibabu yake ambayo yamefikia asilimia 90 kabla ya kurejea uwanjani kuipambania timu yake hiyo katika msimu huu 2023/24.
Manula yupo nje ya uwanja tangu katikati ya msimu uliopita akiuguza maumivu ya nyama za paja kabla ya kupelekwa Afrika Kusini hivi karibuni kufanyiwa operesheni.
Kurejea kwa kipa huyo, kutaongeza ushindani mkubwa katika nafasi hiyo ya golini mbele ya kipa kutoka Morocco Ayoub Lakred aliyesajiliwa katika usajili wa msimu huu kama mchezaji huru.
Kipa huyo amesajiliwa kuja kumpa changamoto ya ushindani, Manula ambaye amedumu katika kikosi cha kwanza ndani ya misimu minne hadi mitano mfululizo akiwa na Simba SC.
Daktari Mkuu wa timu hiyo, Edwin Kagabo amesema kuwa kipa huyo hivi sasa anaendelea na mazoezi ya binafsi ya uwanjani kidogo na gym.
Kagabo amesema kuwa kipa huyo anatarajiwa kurejea uwanjani mwishoni mwa Agosti, mwaka huu ambapo ataanza mazoezi magumu ya pamoja na wenzake.
‘Manula hali yake inaendelea vizuri ambapo matibabu yake yamefikia asilimia 90 kwa sasa, hivi sasa yupo chini ya uangalizi mkubwa wa madaktari akiendelea kufanya mazoezi ya binafsi ya gym na uwanjani kidogo.
“Hivyo mwishoni mwa mwezi huu Agosti, anatarajiwa kuungana na wachezaji wenzake kufanya mazoezi magumu ya kitimu kujiandaa na michezo ya msimu huu,” amesema Kagabo.