Rasmi Mlinda Lango chaguo la kwanza wa Simba SC, Aishi Manula ameondolewa katika mipango ya mechi za hatua ya Robo Fainali ya mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika kutokana na afya yake kutokuwa imara, imefahamika.

Simba SC inatarajia kuikaribisha Wydad Casablanca kutoka Morocco katika mechi ya kwanza ya hatua ya Robo Fainali Afrika itakayochezwa kesho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.

Manula aliumia nyonga katika mechi ya Robo Fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ iliyochezwa juma lililopita dhidi ya Ihefu ya Mbeya na kupelekea mchezo uliofuata, timu hizo zikikutana tena kwenye Uwanja wa Highland Estates siku tatu baadaye, kipa chaguo la tatu, Ally Salim, alisimama langoni.

Taarifa zilizopatikana jijini zinasema Manula hayuko kambini na amepewa mapumziko ya muda wa wiki mbili ili kuuguza maumivu yake.

“Manula hayuko kambini, na kama maumivu yake yataendelea, basi atafanyiwa upasuaji, kwa sasa amepewa ruhusa ya wiki mbili,” kilisema chanzo chetu.

Chanzo hicho kiliongeza Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Olivieira Robertinho’ juzi jioni alifanya kikao na wachezaji wakongwe wa timu hiyo ili kuweka sawa sintofahamu iliyopo kuhusu  nani atasimama langoni baada ya Beno Kakolanya ambaye inadaiwa haaminiki mbele ya mabosi wa klabu hiyo baada ya kubainika amesajiliwa na Singida Big Stars kwa ajili ya msimu ujao.

Chanzo chetu kilisema Kakolanya na Salim wameendelea kufanya mazoezi vizuri kwa ajili ya kuwakabili Waarabu hao nyumbani na ugenini baada ya wiki moja.

Hata hivyo Kakolanya amesema anaendelea vyema na mazoezi na siku zote amekuwa akiheshimu uamuzi wa benchi la ufundi ambalo huamua nani anaaanza katika kila mchezo.

“Mimi ninafanya mazoezi kama kawaida, ila mpaka muda huu (jana mchana), sijui nani atadaka hiyo Jumamosi, tusubiri wakubwa,” amesema Kakolanya

Naye Mwenyekiti wa Simba SC, Murtaza Mangungu, amesema klabu yao inafahamu ubora wa Wydad Casablanca na ili kufikia malengo, watalazimika kuongeza umakini kuelekea mchezo huo.

Mangungu amesema ukaribu na urafiki waliokuwa nao na Raja Casablanca umewasaidia kuelekea mchezo huo muhimu na umewaongezea hali ya kujiamini.

“Viongozi kwa kushirikiana na benchi la ufundi tunahakikisha maandalizi yanakwenda vyema, kila idara inatakeleza majukumu hasa ya kimbinu na kiufundi, mipango yetu ni mizuri tangu mwanzo, tunaamini tutapata matokeo chanya, wachezaji wanautayari na wanauzoefu mkubwa kuelekea mashindnao haya, hatuna cha kuogopa,” amesema Mangungu.

Wakati huo huo, mshambuliaji wa Timu ya Soka ya Taifa (Taifa Stars), Simon Msuva, amewaambia Simba wasicheze mpira wa kufanana na Wydad kama wanataka kupata ushindi.

“Simba wanatakiwa kuwa makini nyumbani na kutoingia katika mfumo wa Wydad Casablanca, hii timu imekuwa ikipoteza muda uwanjani na kutafuta sare hasa wakiwa ugenini. Najua kwa kiasi fulani tabia ya timu za Kiarabu ni wajanja, huwa hawatumii nguvu kubwa ugenini,” alisema Msuva.

Kikosi cha Wydad Casablanca kilishawasili nchini tangu juzi kwa ajili ya mchezo huo wa kwanza wa hatua ya Robo Fainali.

Msuva aliwahi kuichezea Wydad Casablanca katika msimu wa 2020/22 kabla ya kutofautiana na klabu hiyo na sasa anacheza soka la kulipwa Saudi Arabia.

Zogo la Lionel Messi laibuka tena La Liga
Wizi Mkubwa: Korea yaidhulumu Sweden Bilioni 774